Wednesday, October 30, 2013

Uozo wa CHADEMA wajulikana...Hapa nimeweka katiba ya mwaka 2004 na 2006....Ukweli ni kwamba, Katiba ya 2006 Ilibadilishwa kinyemela




Kwa siku za karibuni, umezuka mjadala mkali ndani ya mitandao ya kijamii  hasa baada ya Samson Mwigamba ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha kuwatuhumu viongozi wa kitaifa wa CHADEMA kuwa wamebadilisha katiba kinyemela kwa kuondoa ukomo wa uongozi wa awamu mbili ili waendelee kubaki madarakani. 

Mwigamba alitoa shutuma hizo akitumia jina bandia la Maskini Mkulima. Katika shutuma zake Mwigamba alisema yafuatayo;

"Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitanomitano. 

"Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa. 

"Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa nayenye athari zisizomithirika kwa chama.

"Ni muhimu wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti.
"Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi. 
"Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu."

Mara baada ya taarifa hiyo ambayo ilibebwa kwa jina la Wito kwa wana CHADEMA wote! ambayo ilieleza madhaifu ya chama na kubadilishwa kwa vipengele vya katiba kinyemela, Dr Slaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA alitoa ufafanuzi ufuatao;

"Nataka kuwahakikishia wanachadema wote kuwa  nimekuwa ndani ya Chadema kuanzia 1998 ambapo nilikuwa Makamu Mwenyekiti Bara, na baadaye 2003 Kaimu Katibu Mkuu, na hatimaye Katibu Mkuu, hivyo nimeshiriki kikamilifu kuandaa Katiba ya 2004 na pia Katiba ya 2006 baada ya Rebranding ya Chama. 

"Nataka niwahakikishie wanachadema, hakuna toleo lolote la Katiba ndani ya Chadema imeweka " muda wa Uongozi kuwa vipindi viwili tu", kuanzia Katiba aliyoiasisi Mzee Mtei na kupitishwa na Mkutano Mkuu, wala si ya 2004 au ya 2006. 
"Kama kuna mtu anasema ilikuwepo na imeondolewa kinyemela, basi aonyeshe kifungu hicho kwenye Katiba yeyote ile, au miniti za kikao chochote kile."

Hata hivyo, majibu hayo ya Dr Slaa yanaonekana kutofautiana na yale ya JOHN MNYIKA aliposema kuwa kwenye katiba ya 2004 kipengele cha ukomo wa uongozi kiliwekwa lakini hakikuingizwa kwenye katiba ya 2006. John Mnyika anasema  yafuatayo;

"Kuhusu Katiba, nina nakala mango (hard copy) tu ya katiba ya 2004, ilikuwa na kipengele cha vipindi viwili vya nafasi ile ile. Hata hivyo, katiba mpya iliyoandikwa mwaka 2006 haikuwa na kipengele hicho. Hivyo, sio kwamba kimeondolewa kinyemela ila hakikuwepo kwenye katiba mpya. "

Baada ya malumbano hayo, nilifanya utafiti mdogo ili kujiridhisha na hoja zilizotolewa na viongozi hao. Kwa msaada mkubwa kutoka kwa wadau muhimu ndani ya CHADEMA, nimefanikiwa kupata nyaraka zifuatazo

  1. Nakala ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2004 iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza
  2. Nakala ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006 iliyoandikwa kwa lugha ya kiswahili
  3. Muhtasari wa Mkutano Mkuu Maalum wa CHADEMA uliofanyika katika ukumbi wa PTA Dar es Salaam tarehe 13, Agosti 2006

Nitajaribu kuweka vipengele muhimu mahsusi kwa mjadala huu. Nitajikita kwenye hoja moja tu ya Mwigamba kuwa Viongozi wamefanya marekebisho ya katiba kinyemela kwa kuondoa ukomo wa madaraka ili waendelee kuwepo madarakani.
 
Katiba ya mwaka 2004 ipo wazi kabisa katika hoja ya ukomo wa madaraka. Ibara ya 6.3.2 kipengele cha (c) kinasema ifuatavyo; 
''Leaders who finish their term of office can be eligible for re-election provided he qualifies but no leader can hold the same post at the same level of the party structure for more than two terms. 

Kutokana na kipengele hiki, kauli ya Dr Slaa kuwa hakuna katiba ya CHADEMA iliyoweka ukomo wa madaraka ni ya kushangaza ikizingatiwa kuwa yeye ni Katibu Mkuu na hakupaswa kusema uongo mbele ya watu ambao wanaelewa mengi kuhusu katiba hizo.

Katika Mkutano Mkuu Maalum wa mwaka 2006 ambao ulikuwa na ajenda 4 ambazo ni;
  1. Kufungua Mkutano
  2. Maboresho ya Katiba
  3. Maazimio juu ya Katiba Mpya na
  4. Kufunga Kikao

ulijadili vifungu 10 ambavyo vimefanyiwa marekebisho kutoka kwenye katiba ya 2004. Kati ya vipengele hivyo, kipengele cha ukomo wa madaraka hakimo na hii ni kusema kuwa hoja hiyo haikuwa na marekebisho. Vipengele vilivyofanyiwa marekebisho kwa mujibu wa muhtasari huo vimeambatishwa na taarifa hii.
 
Katiba ya Mwaka 2006 ndiyo inayolalamikiwa kuchakachuliwa kwa vile kipengele cha ukomo wa madaraka hakimo na hakuna mkutano uliojadili hoja hiyo. 
 
Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa hoja za Samson Mwigamba ni sahihi na viongozi wa CHADEMA hususan DR WILBROAD SLAA NA JOHN MNYIKA wametoa majibu ya uongo kupinga hoja za kweli. Kwa mantiki hiyo, ni wazi kuwa katiba imechakachuliwa kwa maslahi ya wanaotetea uchakachuaji huo.
 
Hii  ni katiba  ya  2004
 
 
  
Muhtasari wa Mkutano Mkuu Maalum wa CHADEMA uliofanyika katika ukumbi wa PTA Dar es Salaam tarehe 13, Agosti 2006
 
 
 
 

KATIBA YA MWAKA 2006
6.3 Uchaguzi wa Viongozi na Muda wa Uongozi
 
6.3.1 Utaratibu wa Uchaguzi
 
(a) Uchaguzi wa viongozi utazingatia taratibu na sifa za uongozi kama  zilivyofafanuliwa katika kanuni za Chama.
 
(b) Maombi ya uongozi yatafanywa kwa maandishi kwa kujaza fomu maalum  zilizoidhinishwa na Baraza Kuu la Chama.

(c) Majina ya wagombea wote wenye sifa zilizotakiwa yatapigiwa kura za siri na kikao  kinachohusika na mshindi atapatikana kwa uwingi wa kura usiopungua 50% ya wapiga kura halali waliohudhuria kikao cha uchaguzi.

(d) Uchaguzi wa viongozi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee utafanyika  kwa kuzingatia Ibara hii ya Katiba.
(e) Ikiwa katika chaguzi za chama kura za wagombea zinalingana Mwenyekiti atakuwa  na kura ya turufu.
 
6.3.2 Muda wa Uongozi
(a) Kila uongozi uliochaguliwa au kuteuliwa wakati wa uchaguzi mkuu wa Chama utashika wadhifa wake kwa kipindi cha miaka mitano.

(b) Kiongozi aliyechaguliwa au kuteuliwa baada ya uchaguzi mkuu atashika wadhifa wake hadi kipindi cha uchaguzi mkuu kinachofuata.

(c) Kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.

(d) Muda wa uongozi unaweza kufupishwa kama mamlaka iliyochagua au kuteua itaamua hivyo.
(e) Ibara hii itahusu pia viongozi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee wa  CHADEMA.
 
6.3.3 Kurekebisha tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Chama

(a) Tarehe ya uchaguzi mkuu wa Chama inaweza kurekebishwa kwa kusogezwa mbele  kwa muda usiozidi mwaka mmoja toka mwisho wa uhalali wa uongozi uliopo.

(b) Mamlaka ya kufanya marekebisho haya yameachiwa Kamati Kuu

(c) Kamati Kuu ndiyo itapanga tarehe ya uchaguzi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake  na Wazee wa Chama.
 
6.3.4 Kukoma kwa Uongozi
(a) Kwa kiongozi kujiuzulu kwa hiari yake
(b) Kwa kiongozi kuachishwa uongozi au kufukuzwa uanachama
(c) Kwa kiongozi kushindwa kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa masharti ya  katiba, kanuni au maadili ya Chama.
(d) Kwa kufariki
(e) Ibara hii inahusu pia uongozi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee ya  Chama

Imeandikwa  na  Chabruma, jamiiforum

SHARE HABARI HII KWA RAFIKI ZAKO HAPA CHINI==>>

KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU BASI BOFYA "LIKE" HAPO CHINI KUUNGANA NASI KWENYE FACEBOOK.

0 comments em “Uozo wa CHADEMA wajulikana...Hapa nimeweka katiba ya mwaka 2004 na 2006....Ukweli ni kwamba, Katiba ya 2006 Ilibadilishwa kinyemela”

Post a Comment

 

FULL MAUDAKU Copyright © 2011 -- Template created by MAMBOMSETO TEAM -- Powered by MAMBOMSETO TEAM

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter