Sunday, November 03, 2013

Mwalimu akamatwa kwa rushwa ya ngono huko Mara.....Aliizuia barua ya mtihani toka NACTE kumshinikia mwanafunzi amvulie nguo



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara, inamshikilia Mkurugenzi wa Kituo cha Makoye Education Centre kilichopo Nyasho Manispaa ya Musoma, Mwalimu Joseph Makoye, kwa tuhuma za kudai rushwa ya ngono.

Inadaiwa alidai rushwa ya ngono kwa mwanafunzi aliyekuwa akifanya maandalizi ya kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne kwa mwaka 2013 kituoni hapo unaoanza leo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru mkoani Mara, Holle Makungu, ilidai mwanafunzi huyo ambaye jina lake linahifadhiwa, alijiandikisha kufanya mtihani huo kupitia sanduku la posta 216 la kituo hicho, ambapo barua yake ya mtihani kutoka Baraza la Taifa la Mitihani (NACTE) ilipitia katika kituo hicho na ndipo mkurugenzi wa kituo hicho alipotaka apewe rushwa ya ngono aitoe barua hiyo.

Taarifa hiyo ilidai baada ya barua hiyo kupokelewa katika kituo hicho, ilishikiliwa na mtuhumiwa ambaye kimsingi ndiye mmiliki wa sanduku hilo la barua kwa jina la Makoye Education Centre na kushindwa kumpa binti huyo hadi apewe rushwa ya ngono ikiwa ni sharti la kuipata barua hiyo.

Taarifa hiyo ilidai kuwa mtuhumiwa alitoa tahadhari ya kama binti huyo hatatoa rushwa hatoweza kufanya mtihani wake, kwa kuwa asingempatia barua hiyo.

Kutokana na hali hiyo, binti huyo alikwenda kutoa taarifa Takukuru ambapo iliandaa mtego wa kumnasa mtuhumiwa huyo katika eneo hilo Oktoba 2, mwaka huu, saa moja usiku baada ya mtuhumiwa kumpigia simu mwanafunzi huyo na kumtaka aende hapo.

Alisema maofisa wa Takukuru wakiwa katika mtego wao, alifika mtuhumiwa katika eneo hilo kisha kumuita mwanafunzi na kumpandisha katika gari lenye namba za usajili T 697 BNQ kisha kwenda naye katika nyumba ya kulala wageni ya Tedasi iliyopo eneo la Bweri nje kidogo ya Mji wa Musoma.

Alisema walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo katika nyumba hiyo ya wageni kisha kwenda naye nyumbani kwake eneo la Mkendo Kati na kufanya upekuzi na kufanikiwa kuipata fomu hiyo kutoka NACTE.

“Uchunguzi zaidi wa tukio hilo bado unaendelea na utakapokamilika hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo,” alisema Makungu.


Mtanzania

SHARE HABARI HII KWA RAFIKI ZAKO HAPA CHINI==>>

KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU BASI BOFYA "LIKE" HAPO CHINI KUUNGANA NASI KWENYE FACEBOOK.

0 comments em “Mwalimu akamatwa kwa rushwa ya ngono huko Mara.....Aliizuia barua ya mtihani toka NACTE kumshinikia mwanafunzi amvulie nguo”

Post a Comment

 

FULL MAUDAKU Copyright © 2011 -- Template created by MAMBOMSETO TEAM -- Powered by MAMBOMSETO TEAM

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter